Na Mwandishi Wetu.
Habari za muda na wakati huu ndugu mtanzania mwenzangu, awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu ya kuweza kuiona tena siku ya leo, ni matumaini yangu nawe pia ni mzima wa afya kama ungali na matatizo basi Mwenyezi Mungu akupe wepesi katika hilo na urudi katika hali yako ya kila siku. Pili nipeleke pole kwa ndugu zangu wenye tatizo la albinism kwa maswahibu yanayo wakuta kila uchwao, na pia nipende kuwapa neno la tumaini kuwa bado tupo ndugu zao watanzania wengi tunao wapenda na kuwathamini sana na tupo bega kwa bega nao kukemea na kuwasaka wanaowafanyia vitendo hivi vya kinyama vya kuwakata viungo na hata kuwapotezea uhai wao wa thamani.
Kwa kweli ni jambo la aibu katika uso wa dunia kwa mtanzania au hata mtu yeyote kumto binadamu mwenzake mwenye tatizo la albinism uhai au sehemu ya viungo vya mwili wake kwa imani potofu eti ya kutajirika kupitia viungo hivyo, hili siyo jambo dogo bali ni aibu kubwa kimataifa.
Nikiungana na Mheshimiwa raisi wa taifa letu Dkt Jakay Mrisho Kikwete na wadau wengine wa maendeleo na haki za binadamu kwenye mapambano haya dhidi ya ukatili kwa ndugu zetu wenye tatizo hili la albinism nina lazimika kuipaaza sauti yangu kwa ndugu zangu watanzania kuwa "TUSILISINGIZIE JESHI LA POLISI, TUJILAUMU KWANZA SISI WENYEWE" nina lazimika kuipaza sauti yangu hii dhidi ya malalamiko mengi yanayotolewa kwa jeshi letu la polisi ambalo limekuwa likifanya jitihada za dhati kukabili janga hili, ila kwa bahati mbaya wako wanaotupa shutuma ama kwa kujua au kutokujua kwa jeshi letu hili la polisi.
Nikirudi kwenye msingi wa jambo hili watanzania hatuna budi kukumbuka kauli isemayo "ulinzi unaanza na wewe" haileti maana kuwa jamii haiwajui wahusika wa mauaji na ukatili huu kwani ndani ya jamii yetu ndipo walipo waganga wa jadi, watu wenye tatizo la albinism na pia wahusika wa ukatili huu. Kumekuwa na baadhi ya matukio haya kuwahusisha hata watu wa karibu na wahanga hawa wengine wakiwa ni wazazi au majirani zao. je ni kweli jamii inapaswa kulitupia lawama jeshi la polisi? au inapaswa kujilaumu yenyewe kwa matendo haya?.
Tuikumbuke ile dhana ya ulinzi shirikishi, jamii inapaswa kuwatambua kwa idadi watu wenye matatizo haya ya albinism na kuhakikisha ina watupia jicho kila wawekapo hatua yao, wasije wakadhuriwa na watu wenye hila mbaya juu yao. Yapasa jamii itambue kuwa watu wenye tatizo la albinism ni watu kama watu wengine na hakuna uhusiano wowote kati ya watu hawa na utajiri. Katika historia ya dunia hakukuwahi kutokea wala hata kaa atokee tajiri mkubwa eti kwa kumkata binadamu mwenzake mkono au mguu dhana ya utajiri huletwa kwa kujituma katika nyanja na furusa mbali mbali za kiuchumi na siyo kwa imani potofu za kiganga.
Imeandikwa na John Chuwa
Mawasiliano: johnbambino29@yahoo.com
Monday, March 9, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


0 comments:
Post a Comment