Na Mwandishi Wetu
Ni siku ya jumamosi tarehe 28 mwezi wa pili tu ndani ya mwaka wa 2015, majira ya jioni takribani muda wa saa 10:50 jioni nakumbuka nilikuwa na simu yangu aina ya Sony Xperia ndipo niliposikia mlio wa ishara ya kuingia ujumbe wa maandishi sikusita kuinyanyua pale ilipokuwa na kuufungua ujumbe husika. "JAMANI NAOMBA NITOE TANZIA. CAPTAIN KOMBA AMEFARIKI DUNIA MCHANA HUU HOSPITALI YA TMJ. TAARIFA ZAIDI TUTAJUZANA" Moyo ulipiga Paa! kwa mshituko mkubwa nilioupata huku akili ikinituma kutokuamini ujumbe ule.
Haraka nikachezesha vidole vyangu kumjibu yule aliyenitumia ule ujumbe kutaka adhibitishe kile alichoniambia naye hakusita, ghafla nikazidi kupata jumbe mbali mbali zaidi huku nyingine zikitoka vyombo vikubwa na vya kuaminika vya habari nchini ndipo moyo wangu ulipozidi kupata simanzi na majonzi, nami nikaanza wajuza marafiki na jamaa mbali mbali juu ya pigo hili kwa chama na taifa.
Akiwa amezaliwa miaka 61 iliyopita tarehe 18 mwezi wa tatu wa mwaka 1954 kapteni John Komba ameudumu katika sekta na nyanja mbali mbali nchini ikiwa ni pamoja na kulitumikia jeshi la wananchi wa Tanzania tangu mwaka 1978 hadi 1992 alipo staafu akiwa na cheo cha kapteni. mwaka 2005 alichaguliwa na wananchi wa mbinga magharibi kuwa mbunge wao wakimwamini kuwa ni mtu hodari aliyewapigania wananchi wake hadi umauti ulipomfika.
Buriani, buriani chama na taifa vimempoteza mpambanaji muhimu kapteni John Damiano Komba, ni nani leo hii atakayetufariji kwa nyimbo za kutia nguvu pale tutapokutana na majonzi na simanzi kubwa hapa nchini? nakumbuka sana nyimbo nzuri zenye bashasha kuu za kukienzi chama cha mapinduzi tena zinazopendwa na kila mtu hadi upinzani wapi tutazipata tena?, zile nyimbo za kumnadi mgombea uraisi zenye sauti nzuri iliyojaa furaha na ishara ya ushindi wapi tutazipata tena?, tunaweza sema zipo kwenye CD, Kanda hata maktaba za chama na taifa lakini bado tutazikosa zile ambazo zingeendana na jina la mgombea na wakati husika hakika hili ni pigo kubwa.
Sikupata kuijua vyema historia ya kale ya mpambanaji huyu mahiri katika siasa za chama na taifa ila mbio zangu za kupenda kumjua zaidi ziliongezwa na mambo mengi ila leo nitagusia ujuzi wake katika kutunga na kuimba nyimbo za chama na zilizolihusu taifa. Ile nyimbo yenye mafunzo tele inayoimba "Mgeni kwetu ameingiaa! Mgenii mgeni ii mgeni huyu ni nani!?" uwimbo uliolihasa taifa juu ya uwepo wa ugonjwa hatari wa ukimwi, kila mtanzania aliyekuwa na uwezo wakukariri mambo aliweza kuikariri hii nyimbo, nakumbuka sana enzi hizo nikiwa shule ya msingi Mwereni Manispaa ya Moshi nilikuwa nikiimba mara niisikiapo radio one nikijiandaa kuwahi shule bara barani nitakuwa nairudia rudia huku nikikimbia hakika mwenyezi Mungu alimpa kipaji cha pekee.
Ni ukweli usiopingika sanaa ni moja ya nguzo muhimu katika kuelimisha jamii pia katika kupasha habari juu ya jambo au kitu. Kipindi taifa limempoteza mhasisi wake hayati baba wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ni kapteni Komba aliyetutia nguvu na faraja kwa nyimbo zenye kusisimua na kufariji taifa na dunia kwa kumpoteza mtu muhimu Mwl. J. K. Nyerere. Nani asiyeikumbuka ile nyimbo iliyoimba "Omary Ali Juma!! umemwacha Mkapa na nani?, jana tulikuwa nawe babaa!" hakika mtanzania huyo alikuwa angali mdogo sana wakati makamu wa raisi Dkt. Omary Ali Juma alipotutoka, hakika taifa tumempoteza mpambanaji muhimu.
Zile nyimbo zenye shamra shamra na tumaini kuu la ushindi wa chama cha mapinduzi katika chaguzi mbali mbali uliweza kuzitunga na kuziimba kwa ustadi wa hali ya juu naukumbuka ule wimbo wa "ccm!! ccm!! aah!! aah!! chama cha mapinduzi ccm namba wani... na majirani wanajua ccm namba wani, na wapinzani wanajua ccm namba wani" wimbo unaohimiza kupata ushindi katika chaguzi hakika hii ni nguu tosha. Ni wiki chache zimepita tangu tusikie wimbo wa mwisho wa kapteni pale chama kilipotimiza miaka 38 akisisitiza wanachama kudumu ndani ya chama pale aliposema "Hatumwi sumu, hatu jinyongi!, ccm mbele kwa mbele, tumeipenda wenyewe, chaguo letu milele..." hakika umetuachia hadhina kubwa taifa na chama.
Taifa litazidi kukukumbuka sana kapteni John Damiano Komba, Tulikupenda ila Mwenyezi Mungu amekupenda zaidi, buriani! buriani! buriani! kapteni Komba umetuacha na nani?
Imeandaliwa kwa msaada wa mtandao
Mwandishi John B. R. Chuwa.
Mawasiliano: johnbambino29@yahoo.com
Monday, March 2, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


0 comments:
Post a Comment